WAZEE WA KATIBA MPYA MPO NA JAZBA ZENU?

Inaelekea siku hizi ili kuthibitisha msimamo wako ni lazima ukasirike, uanzishe vurumai, na kupandisha mori.

Siasa zetu siku hizi zimekuwa za kuchochea hasira na munkari usioeleweka mwanzo wake. Wenye dhamana ya kutuliza mori nao hupandisha mori, mitaani hakukaliki wala hakulaliki.
Siku hizi wenye kukunja nyuso zao kwa jazba ambazo huumba mistari mithiri ya upinde wa mvua wanaelekea kuteka jamii ati kwamba wajuvi.

Watu wanadhani kuwa tabia za ubedui ndiyo inadhihirisha kwamba wewe ni jogoo unayeyajua kuliko wale waliokaa kimya ama wanaofuata taratibu madhubuti kwa suala husika.

Ugangwe ni mzuri kwa mwenye busara, lakini siyo kila kitu kinahitaji uwe gangwe ndiyo ueleweke. Inawezekana ukawa mwehu kudai kitu mithiri ya mwehu, lakini wehu huo una busara zake ambazo unakuondoa katika jopo la wehu halisi mitaani.

Sote tunatambua katiba ni mali yetu na ndiyo inayojenga msingi wa nchi yetu. Tunajua kuwa kila katiba inapohitaji marekebisho ama kubadilishwa zipo taratibu za kufuatwa ndiyo maana tumeona Mbunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo (chadema), John Mnyika amewasilisha hoja yake rasimu ya katiba mpya kwa katibu wa bunge la jamhuri ya muungano.

Mbunge John Mnyika amefuata taratibu wala hajapandisha mori kuonyesha anahamu sana na katiba mpya.
Hii ni busara na taratibu zinazopendeza watu wote. Na hamu yake inakuwa katika utaratibu wenye uchochezi kifikra kwakuwa tayari ameueleza katika njia halali.

Ndiyo, tunajua kuwa madai ya katiba mpya siyo mageni na hayataisha leo kwakuwa jamii inabadilika na kila mmoja anapenda kujipendelea kwa lolote lililopo.

Kila mmoja anatambua haki ya kuwa huru na kufanya mambo bila kuvunja katiba. Kila mmoja anaweza kushiriki siasa, lakini hakuna maana ushiriki huo uambatane na ngumi ama mateke.
Kwamba kufanya hivyo ndiyo unadhihirisha umwamba wa madai yako. Dai haki yako kwa utaratibu unaoleweka.

Dai katiba mpya ukitofautisha na kudai kitumbua cha chai ulichodhulumiwa nyumbani.
Kulinganisha madai ya katiba mpya na kudai andazi nyumbani ni mantiki iliyopinda. Kudhani maguvu yanaweza kuzalisha katiba mpya mimi naamini tunakosa uelewa juu ya kusimamia madai.

Usilinganishe kudai kalamu ya wino uliyoibiwa shule na suala la katiba mpya.
Kama mkeo anavuruga bajeti ya nyumba basi panga njia halali ya kudai mabadiliko, kumzaba ngumi na mateke haisaidii kitu. Ni sawa na dai hili la katiba, tuidai kwa adabu hata kama ni laiki yetu.

Hili ni sawa suala linalojitokeza sasa kuwa kudai katiba mpya ni lazima watu kuanza kutoana ngeu. Huu ni utaratibu wa kihuni, tunataka njia muafaka ya kuwasilisha madai yako.
Sidhani kama huyo mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu Luis Moreno Ocampo anaweza kuruhusu kupokea madai ya katiba mpya Tanzania kwa kutishwa kung’olewa meno. Hatuhitaji ngumi wala mateke.

Watu wenye akili zao, na wenye kuelewa kabisa utaratibu wa kudai katiba mpya wanaamua kuanzisha zogo la kutoana ngeu na kung’oana meno.
Hili siyo jambo zuri, maana tunajua kila zuri lina dosari zake. Nimebahatika kuisoma na kuzielewa katiba zote mbili yaani ya Jamhuri ya Muungano na katiba ya Zanzibar.

Nakiri ipo dosari ambazo nachelea kuainisha kwakuwa siyo mtaalamu wa sheria. Lakini ipo dosari moja rahisi mno ilifanyika mwaka 1994 ya kuondoa kipengere cha makamu wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye alikuwa pia rais wa Zanzibar.

Kwa maoni yangu hatukupaswa kukiondoa kipengere hicho kwakuwa kinaonesha umuhimu mkubwa sana wa kuuthamini muungano wetu. Kuondolewa kipengere hicho kinadhorotosha muungano wetu na mshikamano uliopo.

Pamoja na dosari hizo kujitokeza, lakini bado sijaona sababu ya kudai katiba mpya kwa msingi wa mangumi na mateke.
Tumeona wafuasi wa chama cha wananchi (CUF) wakiandamana kudai katiba, tumeona mikogo mingi na harara za kudai katiba mpya inashamiri.

Mikusanyiko na mijadala juu ya katiba mpya inafanyika kwa kutazamana usoni, kama hujashiriki katika kampeni ya kudai katiba kwa munkari basi unacharazwa mangumi na mateke.

Sijui huu ni utamaduni wa aina gani, na sijui kwamba ukiwa na hasira zako juu ya katiba mpya ndiyo utaeleweka sana au la.
Maandamano haya yamekuwa wakiwafanya Polisi wawe makini na uendeshaji wake. Natambua kwamba suala la katiba ni letu sote na linaihusu nchi yetu.

Lakini hakuna sababu ya msingi kutwangana makonde na kuchaniana mashati kwasababu ya kudai katiba. Sote tunahitaji kujenga hekalu moja, hivyo, basi tubomoe mlango huo kwa hekima.

Tunaruhusu Polisi kuvurumisha mabomu ili kutuliza jazba za waandamanaji wa kudai katiba mpya wakati hakuna sababu yeyote ya kudai katiba kwa mijeledi.

Utamaduni wa kudai kila kitu kwa mikwaruzano unashamiri, wapo wenye madai ya msingi lakini namna uwasilishaji wa vilio vyao na kwakutumia ngumi, mateke na mikwaju wanadhani wataeleweka.

Narudia tusiige utamaduni wa ngumi na mateke kufanikisha azma zetu. Kati ya waandamanaji hawa ukiuliza unaijua katiba hiyo unayoikashifu, hana jawabu.

Je unaifahamu kiasi gani katiba inayoongoza nchi hii na ambayo unaambiwa ina viraka? Hakuna mwenye jawabu bora labda kwa wale waliofanikiwa kuzisoma na kuelewa.

Hata hivyo makundi ya waandamanaji wengine wa kudai katiba hususani yaliyofanywa na CUF wapo watoto wadogo waliojiingiza katika maandamano hayo. Sina mashaka walikuwa wanafunzi.

Hawa tunawafundishi njia ya kudai haki(?) ni kwa maandamano, utamaduni huu ukimea unazaa taifa la waandamanaji. Tunawajuza kudai haki kwa kupigana makonde, kutoana ngeu na kadhalika.

Dhima ya kudai haki ni kuhitaji mabadiliko kwa mujibu wa nyakati zetu na zijazo lakini ni muhimu kuelewa kuwa azima ya kudai haki ni kuweka mambo sawa. Kwahiyo usawa huu unapaswa kuenenda utaratibu unaoeleweka.

Vuguvugu la kudai katiba halimaanishi nyote mkunje ngumi na kurusha kwa wengine au kuwatoa mkuku wengine ili washiriki madai haya. Kila mmoja anapima kwa nafasi yake, anachanganua,anaafiki kuwa madai haya ni halali.

Na anayasimami kwa uhalali wala havurumishi ngumi au teke kwa mdaiwa. Bali simamieni hoja kwa utulivu, tuepuke tabia za amri. Na katiba yetu inakuja kwa namna tutakavyotaka. Amani iwe kwenu nyote

Post a Comment

0 Comments