Maafisa wa michezo wauawa Somalia
Wajumbe wa Kamati ya Olimpiki ya Somalia na viongozi wa chama cha
kandanda cha Somalia ni miongoni mwa watu saba waliouwawa katika
shambulio la bomu mjini Mogadishu.
| | | |
Wanaharakati wa kundi la al-Shabab wanasema ndio waliotekeleza shambulio hilo.
Jeshi la kuweka amani la Muungano wa Afrika
nchini Somalia limelaani shambulio hilo kua ni kitendo
"kinachokirihisha" na kusema hakitavuruga juhudi za amani.
Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Somalia , Aden
Yabarow Wiish, na mkuu wa shirikisho la kandanda nchini Somalia , Said
Mohamed Nur, nao pia waliuwawa. Walikua ni miongoni mwa kikundi cha
wageni mashuhuri waliokusanyika kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa
kwa kituo cha televisheni ya taifa ya Somalia.
Rais wa shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA ,Sepp Blatter, alisema ameshtushwa sana kwa vifo vya maafisa hao wa michezo.
Waandishi habari watatu wa kituo cha televisheni
cha Somalia nao pia walijeruhiwa kwa mujibu wa rubaa zilizoiarifu idhaa
ya Kisomali ya BBC.
Jumba hilo la tamthilia lilifungwa katika miaka
ya mwanzo ya 1990 wakati Somalia ilipotumbukia katika vita vya wenyewe
kwa wenyewe na lilifunguliwa upya mwezi mmoja tu uliopita wakati wa
awamu mpya ya matumaini ya kurejea amani.
Waziri mkuu Abdiweli alisema mwanamke aliyejitoa mhanga ndie aliyefanya shambulio hilo.
Akilaani kundi la al-Shabab, alisema ni kawaida yao "kuwaua watu wasio na hatia ".
Salah Jimale,aliyeshuhudia shambulio hilo
ameliambia shirika la habari la Associated Press " Mlipuko huo ulitokea
wakati wapiga muziki walikua wakiimba huku wakishangiliwa na watazamaji.
"Moshi mweusi ulitanda kila mahali. Watu
walipiga mayowe na wanajeshi ghafla wakaanza kufyatua risasi katika
lango la kuingia ndani."
Waandishi wa habari waliokuwepo hapo wanasema
watu kadhaa walijeruhiwa na wanaelezea kuona viatu na simu za mkononi
vilivyojaa damu,na viti kulipuliwa vipande vipande na mlipuko huo.
Katika taarifa yake kundi la al-Shabab limesema
ndilo liliohusika na shambulio hilo lakini limezungumzia bomu
lililotegwa badala ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga.
Msemaji wa Al-Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab
ameliambia shirika la habari la Reuters "sisi ndio tuliopanga mlipuko
katika jumba la tamthilia. Tuliwalenga mawaziri na wabunge makafiri na
ndio miongoni mwa maafa ya leo."
Wanaharakati hao walitimliwa kutoka Mogadishu na wanajeshi wa Muungano wa Afrika mnamo mwaka jana.
Tangu wakati huo kumekuwepo na kipindi cha
utulivu kiasi ambapo shughuli za michezo zilianza upya,mikahawa
kufunguliwa pamoja na jumla la taifa la tamthilia.
Lakini al-Shabab imeendelea kushambulia mji mkuu kwa mabomu na makombora. .
Wakati huo huo,mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Somalia, Augustine Mahiga ameelezea
kukerwa kwake na shambulio hilo katika Jumba la Tamthilia la Kitaifa |
0 Comments