Mwakyembe: Sijafa, nitabaki hai

Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akiingia kwenye ofisi za wizara hiyo tayari kuanza kazi jana na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari. Dk. Mwakyembe, alirejea nchini Ijumaa iliyopita

















Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema waliokuwa wanataka kuandika kichwa cha habari kuwa amekufa sasa wajue yuko hai, na ametaka mjadala kuhusu kuugua kwake ufungwe kwa sababu umekuwa unaiumiza na kuiathiri sana familia yake.
Alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa katika makao makuu ya Wizara ya Ujenzi, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuripoti ofisini kwake kuendelea na kazi baada ya afya yake kuimarika kutokana na kuumwa kwa miezi kadhaa.
Dk. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela (CCM), aliingia ofisini kwake jana saa 3.57 asubuhi na baadaye kuzungumza na waandishi kwa dakika zisizopungua 10, kuanzia saa 4.20 asubuhi.
Alisema mjadala kuhusu kuugua kwake, umekuwa ukishupaliwa na baadhi ya magazeti kwa kuupamba kwa vichwa vizuri vya habari ili kufanya biashara.
“Lingine tu ambalo pengine waandishi wa habari niwaeleze, lakini niwaombe vilevile, jamani sasa suala la Mwakyembe kuumwa basi lifike basi mwisho,” alisema Dk. Mwakyembe, ambaye alirejea nchini Ijumaa iliyopita kutoka kwenye matibabu nchini India.
Aliongeza: “Unajua kwenye Journalism (uandishi wa habari) lazima mtu pia ujali hali inayowahusu watu wengine. Nina watoto. Sasa kila siku huyu baba ambaye anategemewa kufa kesho asubuhi hata kama inaleta headline (kichwa cha habari) kizuri kwenu na kuuza gazeti inaumiza.”
“Mliopenda kupata headline (kichwa cha habari) kwamba nimekufa, basi niko hai na nitaendelea kuwa hai. Kwa hiyo nawaombeni jamani yaishe tafadhali, nawaombeni sana,” alisema.
Alisema alikuwa anaumwa, lakini sasa amerudi kutoka nchini humo alikokuwa amekwenda kupata matibabu akiwa mzima na anaendelea na kazi.
“Nilikuwa naumwa, kwa kweli nimerudi sasa mimi ni mzima kabisa, naendelea na kazi, mmenikuta ofisini kwangu. Na sasa hivi ningependa nifanye kikao kiwe kifupi zaidi maana nina mafaili lundo yananisubiri kuweza kuyapitia,” alisema Dk. Mwakyembe.

AWASHUKURU JK, MAGUFULI, WATANZANIA
Aliishukuru serikali, hasa Rais Jakaya Kikwete, kwa kubeba jukumu hilo hadi kwenda kumuona nyumbani kwake na kushinikiza apata matibabu haraka iwezekanavyo.
Pia aliishukuru serikali kwa kuhakikisha amepata usafiri uliomuwezesha kwenda hospitali nchini India.
Vilevile, alimshukuru Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Katibu Mkuu, Balozi Herbert Mrango na Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk. John Ndunguru, kwa kuendesha wizara peke yao bila msaada wake.
Kadhalika, aliwashukuru wananchi wote nchini, wakiwamo Wakristo na Waislamu, waliojitolea kumuombea apate afya njema.
“Maombi yao hayakuwa ya bure, yamezaa matunda, mimi sasa hivi ni mzima na naendelea na kazi,” alisema Dk. Mwakyembe.


Akijibu swali kwamba uchunguzi wa madaktari umeonyesha alikuwa akisumbuliwa na tatizo gani, alisema anaiachia serikali kupitia tume iliyoiunda kueleza suala hilo.  



“Kwa sababu nilipokuwa India nikaambiwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ameunda tume inachunguza. Tuiache serikali. Kwa hiyo, kama kuna lolote ninalo nitaieleza serikali, na kama kuna taarifa yoyote nitaipa hii tume ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani amesema,” alisema Dk. Mwakyembe.

AWATAKA WAPIGAKURA KYELA
KUSITISHA MAANDAMANO

Aliwashukuru wapigakura wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, ambao walipanga kuandamana kwenda jijini Dar es Salaam kumuona Rais Kikwete ili waelezwe maradhi yaliyokuwa yanamsumbua Dk. Mwakyembe.
“Kwanza nitangulie kwa kuwashukuru sana. Kwanza kwa maombi yao na vilevile subira kubwa waliyokuwa nayo katika kipindi chote ambacho mbunge wao nimekuwa sipo,” alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza: “Naomba niwahakikishie tu wana Kyela hawana haja ya kuandamana tena, nimekuja. Napanga kwenda Kyela mimi mwenyewe katika wiki moja mbili zijazo kufuatana na lundo la kazi litakalopungua hapa wizarani.”
Kuhusu kupishana kauli kati yake na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa hawezi kurejea tena suala hilo kwa vile linashughulikiwa na serikali.
“Serikali imeamua kulichunguza hili suala. Sasa hatuwezi kuendesha parallel systems (mifumo sambamba). Serikali inachunguza halafu sisi huku kama waandishi wa habari tunaongea haya, haitokuwa sahihi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza: “Tuiache serikali iangalie hili suala, maana nikisema serikali ni pamoja na hata yeye DCI Manumba, polisi wote wanahusika. Kwa hiyo, hebu tuipe nafasi serikali ije na taarifa ambayo pengine itaturidhisha wote.”
“Lakini kwa upande wangu mimi kama Mwakyembe, mimi kama nilivyosema siku nyingi namuachia Mungu. Na tuiachie serikali.”

‘UGONJWA WAKE NI WA KITAALAMU’
Alisema hawezi kuwaeleza Watanzania ugonjwa unaomsumbua hawataelewa kwa sababu ni mambo ya kitaalamu.
“Hata kama watu watakimbilia kuuangalia (ugonjwa huo) kwenye kamusi hawawezi kufanikiwa kupata chochote,” alisema Dk. Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9, mwaka jana, yalimlazimu kupelekwa katika Hospitali ya Appolo, India kwa matibabu zaidi.
Maradhi hayo yalizua utata mkubwa baada ya kudaiwa kuwa yametokana na kuwekewa sumu, huku kukiwa na kauli mbalimbali zinazotofautiana kutoka kwake na baadhi ya watendaji wengine wa serikali.
Kauli tata zaidi ziliibuka baada baadhi ya viongozi, akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, kudai kuwa maradhi yanayomsumbua Dk. Mwakyembe yametokana na kulishwa sumu.
Hata hivyo, Kamishna Manumba alijibu madai hayo aliposema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Dk. Mwakyembe hajaugua kwa sababu ya kulishwa sumu na kutishia kuwachukulia hatua waliotoa kauli hizo.
Ripoti ya uchunguzi aliyoisoma Manumba katika mkutano wake na waandishi wa habari Februari 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, inaonyesha kuwa Dk. Mwakyembe hakulishwa sumu huku akisema kwamba pia ilijumuisha taarifa kutoka hospitalini India ambako alikuwa anatibiwa.
Alisema uchunguzi huo unalipa Jeshi la Polisi picha kuwa waliotoa taarifa hizo hadharani wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baada ya kauli hiyo, Dk. Mwakyembe aliibuka na kutoa kauli nzito iliyoonekana kumjibu Kamishna Manumba akielezea kushangazwa kwake na majibu hayo, huku akisisitiza kuwa madaktari waliokuwa wakimtibu walikuwa wakitafiti chanzo cha  ugonjwa wake na walikuwa hawajafikia hitimisho, hivyo si sahihi kwa Manumba kusema kuwa hautokani na kulishwa sumu, kwani sumu si lazima ikudhuru kwa kulishwa tu.
Mbali ya Dk. Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa nyakati tofauti walikana kuijua ripoti hiyo ya Kamishna Manumba.
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kudhamiria kuchukua hatua, Kamishna Manumba aliwasilisha jalada la mashtaka kwa watu hao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, ambaye alithibitisha kupokea jalada hilo, lakini alisema ni vigumu kufahamu ni lini atakapopeleka mahakamani jalada la kesi dhidi ya watu hao.

Post a Comment

0 Comments