SERIKALI imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu, Charles Ekelege, ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Mkurugenzi huyo anakabiliwa na tuhuma za kuanzisha kampuni hewa za
ukaguzi wa magari nje ya nchi hususani, Hong Kong na Singapore na
kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah Kigoda
alithibitisha hayo jana alipokuwa anaelezea mikakati yake mipya ya
kiutendaji tangu ateuliwe na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wizara hiyo
hivi karibuni, akichukua nafasi ya Dk Cyril Chami.
“Kashfa ya TBS ni moja ya sababu za kupanguliwa kwa wakuu wa wizara,
hivyo kwa kuanzia, nimeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TBS kumsimamisha
kazi Ekelege ili kupisha uchunguzi ndani ya shirika hilo,” alisema Dk
Kigoda.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya TBS, Oliver Mhaiki
alipoulizwa juu ya taarifa hizo, alisema hajapokea maagizo ya Waziri.
Aliongeza kuwa, katikati ya wiki ijayo kutakuwa na kikao cha dharura cha
Bodi kuzungumzia mambo kadhaa yanayohusu utendaji wa shirika hilo.
“Mara tukipokea taarifa rasmi juu ya suala hilo kutoka wizarani, tutaliingiza katika ajenda zetu za kikao,” alisema.
Sakata la kuwapo kampuni hewa za ukaguzi wa magari liliibuliwa na
ripoti iliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), pia wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika
ya Umma (POAC) inayoongozwa na Kabwe Zitto na ya Hesabu za Serikali
(PAC) ya John Cheyo.
Hata hivyo, taarifa za ripoti hizo zilionekana kutofanyiwa kazi,
hivyo kuibuliwa kwa tuhuma kuwa Dk Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu
kuwa walikuwa wanamkingia kifua Ekelege kutokana na kushindwa
kumchukulia hatua.
Suala la Ekelege na mengine ya mawaziri na viongozi wa mashirika ya
umma walioguswa na kashfa mbalimbali katika ripoti ya CAG, yaliibua
mjadala mkali katika Bunge la Aprili, kiasi cha baadhi ya wabunge kuweka
kusudio la hoja ya kutokuwa na imani na Serikali, huku wakimtaka Waziri
Mkuu Mizengo Pinda ajiuzulu.
Hatua hiyo ilitokana na kilio cha wabunge na wananchi kutaka
mawaziri na watendaji katika mashirika ya umma wanaoguswa na tuhuma
wajiuzulu, kuonekana kutopewa uzito.
Lakini siku chache baadaye, Rais Kikwete, baada ya kupokea ripoti ya
kilichotokea bungeni na uzito wa tuhuma, alitumia busara za kupanga
upya safu yake ya mawaziri, huku wengi walioguswa wakiwekwa kando.
Hao ni pamoja aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Ezekiel
Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk
Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na
Biashara) na Omar Nundu (Uchukuzi).
0 Comments