Breaking News; wathibitisha kumuua Gaddafi
*Mwili wake wawekwa msikitini
WAPIGANAJI wa Majeshi ya Baraza la Mpito la Libya (NTC) wamethibitisha kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo. Akizungumza na vyombo vya habari muda huu nchini Libya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mahamoud Jibril amesema Kanali Muammar Gaddafi amekufa muda mfupi baada ya kukamatwa na majeshi NTC kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata katika mapambano.
Amesema Gaddafi ameuwawa mjini Sirte baada ya mapambano makali na wafuasi wa kiongozi huyo, ambao idadi kubwa wanashikiliwa na vikosi vya majeshi ya NTC. Askari wapiganaji wa NTC wamekuwa wakisherehekea kwa kufyatua risasi hewani ovyo ikiwa ni ishara ya kujipongeza kwa ushindi.
Akizungumza na vyombo vya habari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Bun Ki Moon amesema umoja huo utakuwa tayari kuisaidia Libya kurejea katika hali yake mara baada ya kuwa huru. “Kifo cha Gaddafi ni historia ya ukombozi kwa nchi ya Libya…UN ipo tayari kuisaidia Libya kipindi hiki,” alisema Moon.
Taarifa zinadai mtoto mwingine wa Gaddafi Motasin naye amekutwa amekufa katika mapambano hayo. Katika mitaa mbalimbali ya nchini Libya wananchi wameonekana kusherehekea ikiwa ni pamoja na kupandisha bendera ya utawala wa NTC tangu taarifa za kifo cha Gaddafi kitangazwe. Ameongoza Libya tangu alipompindua Mfalme Idris I, katika mapinduzi yasiyo ya kumwaga damu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 27.
Maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa, na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa, kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.
Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am na hapo Umoja wa Mataifa ukaondoa vikwazo dhidi ya Libya.
Baada ya miezi kadhaa, serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za magharibi. Hapo ndipo mabadiliko halisi yalionekana kwa kuwa nchi hizo za magharibi zilibadili mtazamo wao na kuacha kumtenga Gaddafi na kushirikiana naye hata kama alikuwa hatabiriki.
Ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar mtaalam wa siasa za Libya. Lakini ni mwanasiasa mashuhuri; hakuna shaka lolote kuhusu hilo. Ni mwanasiasa anayeweza kuhimili misukosuko ya kisiasa kwa hali ya juu sana.’ Muammar Gaddafi alizaliwa jangwani karibu na Sirte mwaka 1942.
Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri na, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.
Gaddafi alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi na aliwahi kupata mafunzo zaidi akiwa Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya, mji wa Benghazi, na kupanga mapinduzi ya tarehe 1 Septemba mwaka wa 1969.
Ghaddafi alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
0 Comments