MJADALA wa mapendekezo ya kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wa umma, wiki hii uliendelea kuichanganya Serikali ambayo ilitoa kauli inayokinzana na msimamo wa CCM na mpango wa miaka mitano wa maendeleo wa Taifa uliopitishwa na Bunge mapema wiki hii.
Mjadala huo ulitua rasmi bungeni Jumatano iliyopita, kupitia hotuba ya Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe, aliyesisitiza katika bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani kuwa kufutwa kwa posho hiyo ni suala la lazima na kwamba, kufanya hivyo, Serikali inaweza kuokoa kiasi cha Sh987 bilioni.
Kauli ya Zitto ilikuwa ikithibitisha ahadi ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye awali aliweka bayana kuwa mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni ni kufutwa kwa posho zote za vikao kwa watumishi wa umma.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo Alhamisi, alitetea malipo ya posho hizo akisema haziepukiki, kauli inayotofautina na iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliyesema suala hilo linajadilika.
Kauli ya Pinda pia inatofautina na ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji (TBC), alisema suala la kupitiwa upya mfumo wa malipo ya posho, ni agenda ya Serikali.
Akijibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), kuhusu suala la posho, Pinda aliwaponda wabunge wa Chadema kwamba wanalikuza jambo hilo ili waonekane wazalendo mbele ya umma.
Lakini msimamo wa Pinda unatofautina na uliotolewa na Nape katika vyombo vya habari, kuwa suala hilo linajadilika na kwamba, si lazima kupinga kila kitu kinachotoka upande wa pili(upinzani).
Mwingine aliyeunga mkono wazo la kufutwa kwa posho ni Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM) ambaye alisema suala hilo ni la kitaifa, lazima lijadiliwe na kupata mwafaka.
Kauli ya Makamba ambaye pia ni Mjumbe wa Sekretarieti ya CCM inaonekana kutofautina na mawazo ya wabunge wengi wa CCM ambao wamekuwa wakiwashambulia wenzao wa Chadema kwamba wanatumia hoja hiyo kujitafuatia umaarufu.
Wengi wapinga
Wasomi na wanaharakati pia wameungana na kambi ya upinzani kuhusu sula hilo na kupendekeza kuwa mfumo mzima wa utawala ufumuliwe.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wiki hii, wadau hao walisema sio tu kwamba wamekerwa na kauli ya Pinda, bali pia mfumo mzima uliokubali kulipwa posho hizo.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuwa tatizo siyo posho, bali ni mfumo mzima wa serikali ulioegemea kwenye ubepari uchwara.
“Dola imejiondoa katika kumiliki rasilimali, kila kitu sasa ni biashara, hata elimu ni biashara ndiyo maana wabunge wanajilipa posho nyingi ili wakanunue elimu yao na watoto wao. Hii ni Jamhuri ya posho tu,” alisema Ally.
Mhadhiri huyo alihoji, “Kwa nini mwalimu mwenye Shahada ya Uzamili alipwe mshahara mdogo kuliko mfanyakazi wa TRA asiye hata na shahada?" alihoji na kuendelea:
"Tujadili mfumo mzima unaowafanya viongozi wa Serikali na wabunge kujilimbikizia posho na mali nyingi.”
Hata hivyo, alisema Waziri Mkuu na wabunge wengine wana haki kutetea posho hizo kwa vile pamoja na kwamba ni tatizo, zipo kisheria.
“Sikushangaa majibu ya Waziri Mkuu Pinda kwa sababu anaujua mfumo na ameutetea. Kinachotakiwa ni kuubadilisha mfumo, siyo posho tu,” alisema Bashiru.
Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya, alipinga posho za wabunge na watumishi wengine wa Serikali akisema zinachukua sehemu kubwa ya bajeti ya nchi.
“Tunaunga mkono hoja ya kuondolewa kwa posho za wabunge na watumishi wengine wa Serikali zilizo nje ya mshahara. Kama wabunge wanalipwa mshahara na posho ya safari bungeni, kwa nini walipwe tena posho ya vikao na semina?” alihoji Mallya.
Mallya alisema suala hilo ni la kikatiba na kusisitiza kuwa limeibuka wakati mwafaka na linapaswa kuangaliwa wakati huu wa kujadili na kuandikwa katiba mpya.
“Posho hula asilimia 30 ya bajeti ya Taifa. Hii ni hatari na inarudisha nyuma maendeleo ya nchi. Inatupasa tuangalie upya mgawanyo wa rasilimali zetu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema posho za wabunge na maofisa wa umma zinasitahili kufutwa.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2008/9 na 2009/10 jumla ya Sh931 bilioni zilitumika kulipa posho na semina kwa wabunge na maofisa mbalimbali serikalini. Posho ya mwaka 2008/9 ilikuwa Sh506 bilioni. Hii ni zaidi ya bajeti ya wizara moja kwa kipindi cha mwaka mzima” alisema Kibamba.
Alisema fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti ya Taifa hazifiki kwenye miradi ya maendeleo na badala yake hutumika katika kulipa posho kwa wabunge na maofisa wa ngazi za juu serikalini.
“Tunachopinga sisi siyo fedha za kujikimu anazopewa Mbunge kwenda kuhudhuria vikao vya Bunge Dodoma, bali ni siting allowance (posho za vikao),” alilalamika Kibamba.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Semboja Haji, aliunga mkono msimamo wa Pinda akisema hiyo siyo hoja kwa sasa kuna mambo mengi ya kuzungumzia badala ya kujadili malipo ya Wabunge.
Stahiki za wabunge
Kwa mujibu wa ripoti ya utendaji wa Bunge la 2005-2010 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wabunge walijiongezea mishahara na posho mwaka 2009.
Kabla ya hapo walikuwa wakilipwa jumla ya Sh7 milioni kwa mwezi na kufuatia nyongeza hiyo wabunge wanalipwa Sh12 milioni huku Sh3 milioni zikiwa zinakatwa kodi.
Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kwa upande wake inaitaka kuharakisha kutunga Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2010, ili sheria hiyo isaidie katika kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma zikiwamo posho za vikao na usafiri.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Abdalah Kigoda akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12 alisema, serikali inatakiwa kuchukua hatua maalumu kuangalia eneo la posho ili liwe njia mojawapo ya kuiwezesha kuongeza mapato.
Lakini wakati hoja hiyo ikipamba moto ndani ya Bunge, ilibainika kuwa CCM kilikuwa kimeanza machakato wa kufuta posho hizo ikiwa ni hatua ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, mkakati ulioanzishwa takriban mwezi mmoja uliopita na sekretarieti mpya inayoongozwa na Katibu Mkuu, Willison Mukama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe wa sekretarieti walihoji uhalali wa posho wanazolipwa hata vikao vinapofanyika katika sehemu ambako ni makazi yao na kwamba hoja hizo ndizo zilizozaa wazo la kufutwa kwa posho katika vikao.
Viwango vya malipo
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili umebaini kuwa malipo ya wabunge yamegawanyika katika sehemu nne; mshahara ambao ni Sh2,300,000 kwa mwezi, posho ya Ubunge kila mwezi ambayo ni Sh5 milioni, posho ya kujikimu (Per-Diem) kwa Sh80,000 wawapo nje ya majimbo yao kikazi na posho ya vikao (sitting allowance) kwa siku Sh70,000 kwa kila mbunge.
Posho ya Ubunge ya kila mwezi ambayo ni Sh5 milioni ni kwa ajili ya mafuta, matengenezo ya gari, malipo ya dereva na wasaidizi wa mbunge.
Kwa maana hiyo, kwa kawaida mbunge hulipwa Sh7.3 milioni kila mwezi kabla ya kukatwa kodi na wawapo Dodoma na Dar es Salaam kwa ajili ya vikao vya kamati na Bunge au mikoani kwa ajili ya kukagua shughuli zilizopo chini ya kamati zao, hulipwa kiasi cha Sh150,000 kila siku; Sh70,000 kwa ajili ya vikao na Sh80,000, kwa ajili ya kujikimu.
Kwa maana hiyo Bunge linatarajiwa kutumia kiasi cha Sh1.788 bilioni kwa ajili ya kugharimia vikao 73 vya Bunge la bajeti iwapo wabunge wote 350 waliopo watahudhuria vikao hivyo.
Kwa hesabu hizo kila mbunge katika mkutano wa Bunge la bajeti anatarajiwa kuondoka na kikita cha Sh5.1 milioni mbali na Sh5.58 milioni ambazo ni malipo kwa ajili ya kujikimu (Per diem), fedha ambazo ni mbali na mshahara wake kwa mwezi na posho ya ubunge.
Vitisho vya Spika
Vita ya kutaka kufutwa kwa posho za vikao ilifikia hatua ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutishia kuwa atatumia kanuni za Bunge kumfukuza Zitto Bungeni kama hatasaini karatasi za mahudhurio.
Kauli ya Makinda inafuatia msimamo wa Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) kukataa posho za vikao na kwamba kwa kuwa kinachohalalisha yeye kulipwa posho ni karatasi za mahudhurio basi hatasaini.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanasema kauli ya Spika inaweza isitekelezeke kwani iwapo Zitto atakuwa akichangia mijadala bungeni na mijadala hiyo kunukuliwa na Hansard (taarifa rasmi za Bunge), huo ni uthibitisho mzuri zaidi kuliko kusaini karatasi.
Makinda amekuwa akisisitiza kwamba hata kama Zitto hataki fedha hizo, wao lazima waziweke kwenye akaunti benki kwani ndivyo sheria zinavyowaelekeza.
0 Comments