{TUNATAKA HAKI ZETU } KAZI KWELIKWELI TANZANIA

MADEREVA wa malori yanayosafirisha mizigo katika Nchi za Maziwa Makuu wametishia kugoma kama  wamiliki wa magari hayo hataingia nao kwenye mikataba ya ajira na Serikali kuwatambua rasmi.

Walidai kwa pamoja madereva hao  wataitisha mgomo wa  nchi nzima baada ya siku 30 iwapo Serikali itashindwa kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo wawapo  safarini na pia kama wamiliki wa magari hayo watashindwa kuingia nao mikataba ya ajira.

Wakizungumza jijini hapa juzi walisema wamevumilia  kwa kipindi kirefu na kwamba kila wanapodai haki zao kwa Serikali na wamiliki wa magari ya mizigo  hawasikilizwi na kusababisha kukabiliwa na hali ngumu kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake , dereva aliyejitambulisha kwa jina la Kiula Msongazila, alisema Wizara ya Ujenzi iweke mizani ya kupimia mizigo bandarini badala ya hivi sasa ambapo ipo Kibaha kwani wamekuwa wakipata usumbufu wa kurudishwa njiani ikibainika mzigo umezidi kipimo na hivyo kusababisha usumbufu kwa madereva.
Naye Fikiri Mohamed, alisema wamekuwa  wakifanya kazi kwa muda mrefu bila ya ajira na badala yake  wanalipwa Sh120,000 kwa mwezi wakati wanasafiri umbali mrefu kwenda katika nchi za Maziwa Makuu.

Wakati huohuo, naye Aidan Mhando anaripoti kutoka Dar es Salaam kwamba madereva wa magari ya mizigo  nchini, wameiomba Serikali  kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukifunga kituo cha kudai fedha eneo la Kibaha Misugusugu ili kuwapunguzia  kero.

Aidha wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukifunga kituo hicho  kutokana na kukithiri kwa usumbufu.
Wakizungumza   kwenye Ofisi za gazeti hili , D ar es Salaam jana madereva hao,  walishanga kuona vituo vya kukusanya kodi kwa magari ya mizigo vinaongezeka kila mahali bila wao kupewa taarifa yoyote.
Madereva hao walidai kwamba eneo hilo ambalo wanatozwa kodi ya Sh 2,000 kila safari kwa madai ni kodi ya uchafuzi wa mazingira  linasababisha kero nyinbgi zikiwemo kukosa huduma za vyoo na  maji.
Mwakilishi wa umoja wa magari ya mizigo, Said Ally alisema mpaka sasa kuna vituo zaidi ya 10 ambavyo kila kituo wanatozwa kodi ya Sh2000 kwa magari zaidi ya 250 kwa siku na kwamba  wanashangaa kuona vinaongezeka vituo vingine bila wao kupewa taarifa yoyote.

“Kila tunapofika katika maeneo ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya magari ya mizigo tunasimama na kukaguliwa pamoja na Sh 2000 katika maeneo hayo, lakini sasa kumeibuka mtindo wa watu kujifungulia vituo kama hivyo wakidai kutumwa na TRA kukusanya kodi ya uchafuzi wa mazingira,”alisema Ally.
Ally aliongeza usumbufu wa kituo hicho ulishawasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania  ambako walikana kukifungua jambo ambalo limezidisha utata wa kituo hicho.



“Madereva wa malori tunanyanyaswa, tumevumilia sana lakini sasa uvumulivu wetu  tunataka ufike mwisho ambapo tunatangaza kuwa baada ya siku 30 kama madai yetu hayatapatiwa ufumbuzi tutagoma nchi nzima,”alisema Mohamed.
Dereva Issa Makame, alisema kitu kingine kinachowasikitisha ni kwamba Dol 500  za Marekani zinazotolewa na wamiliki wa mzigo wanaposafirisha mizigo zimekuwa zikichukuliwa na matajiri (wenye magari) badala ya fedha hizo kuwa mikononi mwa madereva.
Naye Shadrack Edward alizilalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mamlaka ya Usairishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Edward alisema serikali inapaswa kuwatendea haki madereva na kuwaona watu muhimu kwa kuhakikisha taasisi hizo tatu za Serikali zinafanya kazi kwa kushirikiana badala ya hivi sasa ambapo zimekuwa zikiwasumbua.

Post a Comment

0 Comments