YASEMA AJIRA KWA VIJANA SIYO BOMU, WAZIRI KABAKA AMWAGA TAKWIMU, AELEZA MAANA YA AJIRA Geofrey Nyangoro SERIKALI
imetoa takwimu za ajira kwa vijana nchini ikiwa ni majibu kwa kauli za
mara kwa mara za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye
amekuwa akisema tatizo hilo ni kubwa akililinganisha na bomu
linalosubiri kulipuka. Lowassa amenukuliwa katika matukio manne
tofauti kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu, akionya tatizo
hilo la ajira kwa vijana kwamba linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Jana,
Waziri wa Kazi na Ajira alisema tatizo hilo haliwezi kufafanishwa na
bomu na kusema wanaosambaza uvumi huo hawaitendei haki Serikali, kwani
tatizo hilo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 hadi asilimia
11.7, mwaka 2006.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari
uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kabaka alitoa ufafanuzi wa
hali ya ajira nchini na hatua ambazo Serikali inachukua kushughulikia
tatizo hilo. “Hali halisi ya ukuaji wa uchumi nchini ni nzuri lakini,
haiwezi kuonekana kama wananchi wake ni maskini na hawana ajira. Hata
hivyo, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia suala
hilo ikiwamo la kuhimiza uwekezaji nchini,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Kitendo
cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu
linalosubiri kulipuka, siyo kweli na kudai Serikali hayaijafanya kitu
wanakuwa hawaitendei haki.” Alisema utafiti uliofanywa na wizara yake
kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa
tatizo hilo limepungua kwa asilimia 1.2.
Mikakati Waziri
Kabaka alisema utafiti uliofanywa na NBS mwaka 2006 ikishirikiana na
wizara hiyo unabainisha kuwa nguvu kazi ya Tanzania ni 20.6milioni kati
ya watu 37.5 milioni, kwa wakati huo.
Alisema kutokana na utafiti
huo, watu 18.3milioni sawa na asilimia 88.3 ya watu hao 20.6milioni
walikuwa na ajira huku waliokuwa kwenye ajira ya sekta rasmi wakiwa ni
17milioni sawa na asilimia 92.7.
Kabaka alisema katika utafiti
huo, watu 1.3milioni walikuwa kwenye ajira isiyo rasmi huku utafiti
ukibaini kuwa kila mwaka watu 800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye
soko la ajira.
“Utafiti unaonyesha hali ya ukosefu wa ajira
nchini umeshuka kidogo kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 na kufikia
asilimia 11.7 mwaka 2006, hata hivyo kiwango hicho ni cha juu kwa nchi
kama Tanzania ambayo haina huduma za kinga kwa watu wasio na ajira,”
alisema Kabaka.
Waziri Kabaka alisema pamoja na kushuka kwa
kiwango cha ajira, bado kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa huku
kikitofatutiana baina ya kundi moja na jingine akisema Tanzania siyo
kisiwa hivyo, tatizo linaloikumba dunia la ukosefu wa ajira pia
linaikumba nchi hiyo.
Alitaja mikakati ya Serikali kuwa ni pamoja
na utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kukuza ajira ambayo
ni pamoja na mpango wa mafunzo yenye kuwezesha vijana kujiajiri, mfuko
wa maendeleo ya vijana, mpango wa kukuza ajira kwa vijana na mpango wa
uwezeshaji wananchi kiuchumi na kukuza ajira.
Kabaka alitaja
mipango mingine kuwa ni ule wa uwekezaji katika elimu na mafunzo,
kujengea uwezo mamlaka za Serikali za mitaa (LGAs) na ajira za moja kwa
moja zinazotolewa na Serikali kupitia sekta mbalimbali.
“Serikali
imetoa ajira kwa walimu 15,000 wa shule za sekondari na msingi na pia
kwa kipindi cha miaka mitano 2007 hadi 2011, ajira 414,679 zimepatikana
kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC),” alisema Kabaka.
Waziri Kabaka
alibainisha mpango kabambe uliowekwa na Serikali katika kukabiliana na
tatizo la ajira, ambao alisema hadi kufikia mwaka 2015, itakuwa
imepunguza tatizo la ajira kutoka asimilia 11.6 ya mwaka 2006 hadi
kufikia asilimia tano.
Alisema katika kutekeleza hilo, Serikali
imeanza kuchukua hatua na kwamba imeanda programu ya kwanza itakayolenga
kutambua vijana wote wenye taaluma aina ya ujuzi walionao katika kila
wilaya hapa nchini.
“Programu hii ambayo utekelezaji wake
unatarajia kuanza mwaka wa fedha wa 2012/13, imejikita katika kuwatambua
vijana na shughuli zao ili kuwajengea uwezo katika kukuza tabia ya
kijasiriamali, kuwawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kukuza soko la
bidhaa za ndani kwa kuweka mazingira kutumia bidhaa za Tanzania,”
alisema Kabaka.
Alisema pia mpango huo umejikita kuwezesha kijana
mmojamoja au kikundi kujiajiri, vijana wasomi na wenye ujuzi
wanaohitimu katika vyuo vya elimu ya juu kujiajiri na kutengeneza
mazingira ya kuajiri wengine na pia kuwezesha sekta binafsi na taasisi
za umma kuwekeza katika sekta zenye kipaumbele katika kutoa ajira.
Waziri
Kabaka alisema Serikali imejipanga kutekeleza mpango wa kukuza ajira
katika maeneo ya mikoa na wilaya ili kuwezesha kupunguza tatizo la ajira
na kuwafanya vijana wasikimbilie mijini.
Maana ya ajira Akinuuku
tafsiri inayotumika duniani na kutambuliwa na Shirika la Kazi la
Kimataifa (ILO), Waziri Kabaka alisema maana ya ajira ni shughuli yoyote
halali anayoifanya mtu mwenye umri wa kufanya kazi kwa kujipatia kipato
na kwa kawaida shughuli hiyo ni ya hiari inayotambuliwa kisheria na
hufanywa kwa saa 40 hadi 45 kwa wiki.
Alisema ukosefu wa ajira ni
hali ambayo hutokea wakati watu walioko kwenye umri wa kufanya kazi na
ambao wangependa kufanya kazi wanatafuta bila ya kuipata.
“Tafisiri
hii ya kimataifa haiwajumuishi wale wasiotafuta kazi, wasiopenda
kufanya kazi hata kama hawana kazi,” alisema Kabaka na kuongeza: “Lakini
tafisiri inayotumika zaidi Tanzania inatambua wote wasio na kazi na
ambao wako tayari kufanya kazi bila kujali wanatafuta kazi au la na
inawahusisha hata wasio na uhakika wa kufanya kazi hata ya siku moja.” Alitaja aina tatu za ajira ambazo ni kazi ya staha, kazi chini ya kiwango na ajira maskini.
Alisema
ajira za staha ni zile ambazo zina tija kiusalama, heshima haki za
wafanyakazi na kipato cha kutosha, wakati ya ile ya chini ya kiwango ni
ile ambayo haitoshelezi kutumia uwezo, muda na taaluma yote ambayo
ambayo mhusika anayo. Ajira maskini ni ile ambayo kipato kinachopatikana
ni cha chini ya kiwango kisichomwezesha mtu kuishi.
Akirejea
utafiti wa ILO wa mwaka 2010/11, Waziri Kabaka alisema ripoti hiyo
inaonyesha hali ya umaskini na ukosefu wa ajira duniani ni kubwa. Watu
205 milioni dunia kote mwaka 2010 hawakuwa na ajira. Alisema idadi
hiyo ilikuwa sawa na ongezeko la nguvu kazi isiyo na ajira duniani ya
watu 27.7 milioni kulinganisha na ile ya mwaka 2007.
Alisema
sababu za ongezeko la ukosefu wa ajira kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni
kutokana na utandawazi, maendeleo ya mawasiliano, mabadiliko ya
teknolojia ambayo hayahitaji nguvu kazi nyingi katika utendaji kazi na
kudidimia kwa nguvu za kiuchumi hasa katika nchi zinazoendelea.
Lowassa na ajira Novemba
15, mwaka jana akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, Lowassa alionya
kuhusu tatizo hilo na kulitaka lisaidie kujenga vyuo vya ufundi.
Alitoa
takwimu akisema utafiti wa mwaka 2006, ambao hata hivyo, hakusema
ulifanywa na taasisi gani, ulionyesha tatizo hilo kwa sasa limekuwa na
kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa miaka kati
ya 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvukazi ya taifa... “Ninapozungumza hili
siyo nia yangu kumlenga mtu. Mimi ni Yohana Mbatizaji, hii ni sauti
inayolia nyikani.”
Novemba 29, mwaka huo wa jana akiwa harambee
ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKT), Usharika wa Amani
Sabasaba, Singida, Lowassa alirudia tena suala hilo la tatizo ajira.
Mapema
mwaka jana, Lowassa pia alifanya mkutano na waandishi wa habari Mjini
Arusha na kuzungumzia tatizo hilo la ajira ambalo alilifananisha na
bomu.
Jumatatu iliyopita, Lowassa alirejea kauli hiyo alipokuwa
katika sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara
akisema: “Nawaomba maaskofu katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la
tatizo la ajira kwa vijana.... hili kama tulivyosema ni bomu
linalosubiri kulipuka...”
0 Comments