SAUTI YA AFRIKA
TOA MAONI YANAYOJENGA JAMII
March 24, 2012
AIBU SANA!!!
March 23, 2012
UZALENDO
|   | 
| Mfanyakazi wa kampuni ya Clouds Media, Said Bonge 'Bonge' akirekebisha singe kwenye mnara wa askari katika makutano ya mtaa wa Samora na Azikiwe Dar es Salaam jana. Singe hiyo ilikunjwa wiki iliyopita na mtu anayedaiwa kuwa ni mgonjwa wa akili aliyetaka kuiangusha sanamu hiyo inayolitambulisha jiji la Dar es Salaam.(Na Mpigapicha wetu) | 
March 22, 2012
Serikali yamjibu Lowassa >

YASEMA AJIRA KWA VIJANA SIYO BOMU, WAZIRI KABAKA AMWAGA TAKWIMU, AELEZA MAANA YA AJIRA
Geofrey Nyangoro
SERIKALI imetoa takwimu za ajira kwa vijana nchini ikiwa ni majibu kwa kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye amekuwa akisema tatizo hilo ni kubwa akililinganisha na bomu linalosubiri kulipuka.
Lowassa amenukuliwa katika matukio manne tofauti kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu, akionya tatizo hilo la ajira kwa vijana kwamba linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Jana, Waziri wa Kazi na Ajira alisema tatizo hilo haliwezi kufafanishwa na bomu na kusema wanaosambaza uvumi huo hawaitendei haki Serikali, kwani tatizo hilo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 hadi asilimia 11.7, mwaka 2006.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kabaka alitoa ufafanuzi wa hali ya ajira nchini na hatua ambazo Serikali inachukua kushughulikia tatizo hilo.
“Hali halisi ya ukuaji wa uchumi nchini ni nzuri lakini, haiwezi kuonekana kama wananchi wake ni maskini na hawana ajira. Hata hivyo, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia suala hilo ikiwamo la kuhimiza uwekezaji nchini,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli na kudai Serikali hayaijafanya kitu wanakuwa hawaitendei haki.”
Alisema utafiti uliofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo hilo limepungua kwa asilimia 1.2.
Mikakati
Waziri Kabaka alisema utafiti uliofanywa na NBS mwaka 2006 ikishirikiana na wizara hiyo unabainisha kuwa nguvu kazi ya Tanzania ni 20.6milioni kati ya watu 37.5 milioni, kwa wakati huo.
Alisema kutokana na utafiti huo, watu 18.3milioni sawa na asilimia 88.3 ya watu hao 20.6milioni walikuwa na ajira huku waliokuwa kwenye ajira ya sekta rasmi wakiwa ni 17milioni sawa na asilimia 92.7.
Kabaka alisema katika utafiti huo, watu 1.3milioni walikuwa kwenye ajira isiyo rasmi huku utafiti ukibaini kuwa kila mwaka watu 800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira.
“Utafiti unaonyesha hali ya ukosefu wa ajira nchini umeshuka kidogo kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 na kufikia asilimia 11.7 mwaka 2006, hata hivyo kiwango hicho ni cha juu kwa nchi kama Tanzania ambayo haina huduma za kinga kwa watu wasio na ajira,” alisema Kabaka.
Waziri Kabaka alisema pamoja na kushuka kwa kiwango cha ajira, bado kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa huku kikitofatutiana baina ya kundi moja na jingine akisema Tanzania siyo kisiwa hivyo, tatizo linaloikumba dunia la ukosefu wa ajira pia linaikumba nchi hiyo.
Alitaja mikakati ya Serikali kuwa ni pamoja na utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kukuza ajira ambayo ni pamoja na mpango wa mafunzo yenye kuwezesha vijana kujiajiri, mfuko wa maendeleo ya vijana, mpango wa kukuza ajira kwa vijana na mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kukuza ajira.
Kabaka alitaja mipango mingine kuwa ni ule wa uwekezaji katika elimu na mafunzo, kujengea uwezo mamlaka za Serikali za mitaa (LGAs) na ajira za moja kwa moja zinazotolewa na Serikali kupitia sekta mbalimbali.
“Serikali imetoa ajira kwa walimu 15,000 wa shule za sekondari na msingi na pia kwa kipindi cha miaka mitano 2007 hadi 2011, ajira 414,679 zimepatikana kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC),” alisema Kabaka.
Waziri Kabaka alibainisha mpango kabambe uliowekwa na Serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira, ambao alisema hadi kufikia mwaka 2015, itakuwa imepunguza tatizo la ajira kutoka asimilia 11.6 ya mwaka 2006 hadi kufikia asilimia tano.
Alisema katika kutekeleza hilo, Serikali imeanza kuchukua hatua na kwamba imeanda programu ya kwanza itakayolenga kutambua vijana wote wenye taaluma aina ya ujuzi walionao katika kila wilaya hapa nchini.
“Programu hii ambayo utekelezaji wake unatarajia kuanza mwaka wa fedha wa 2012/13, imejikita katika kuwatambua vijana na shughuli zao ili kuwajengea uwezo katika kukuza tabia ya kijasiriamali, kuwawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kukuza soko la bidhaa za ndani kwa kuweka mazingira kutumia bidhaa za Tanzania,” alisema Kabaka.
Alisema pia mpango huo umejikita kuwezesha kijana mmojamoja au kikundi kujiajiri, vijana wasomi na wenye ujuzi wanaohitimu katika vyuo vya elimu ya juu kujiajiri na kutengeneza mazingira ya kuajiri wengine na pia kuwezesha sekta binafsi na taasisi za umma kuwekeza katika sekta zenye kipaumbele katika kutoa ajira.
Waziri Kabaka alisema Serikali imejipanga kutekeleza mpango wa kukuza ajira katika maeneo ya mikoa na wilaya ili kuwezesha kupunguza tatizo la ajira na kuwafanya vijana wasikimbilie mijini.
Maana ya ajira
Akinuuku tafsiri inayotumika duniani na kutambuliwa na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO), Waziri Kabaka alisema maana ya ajira ni shughuli yoyote halali anayoifanya mtu mwenye umri wa kufanya kazi kwa kujipatia kipato na kwa kawaida shughuli hiyo ni ya hiari inayotambuliwa kisheria na hufanywa kwa saa 40 hadi 45 kwa wiki.
Alisema ukosefu wa ajira ni hali ambayo hutokea wakati watu walioko kwenye umri wa kufanya kazi na ambao wangependa kufanya kazi wanatafuta bila ya kuipata.
“Tafisiri hii ya kimataifa haiwajumuishi wale wasiotafuta kazi, wasiopenda kufanya kazi hata kama hawana kazi,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Lakini tafisiri inayotumika zaidi Tanzania inatambua wote wasio na kazi na ambao wako tayari kufanya kazi bila kujali wanatafuta kazi au la na inawahusisha hata wasio na uhakika wa kufanya kazi hata ya siku moja.”
Alitaja aina tatu za ajira ambazo ni kazi ya staha, kazi chini ya kiwango na ajira maskini.
Alisema ajira za staha ni zile ambazo zina tija kiusalama, heshima haki za wafanyakazi na kipato cha kutosha, wakati ya ile ya chini ya kiwango ni ile ambayo haitoshelezi kutumia uwezo, muda na taaluma yote ambayo ambayo mhusika anayo. Ajira maskini ni ile ambayo kipato kinachopatikana ni cha chini ya kiwango kisichomwezesha mtu kuishi.
Akirejea utafiti wa ILO wa mwaka 2010/11, Waziri Kabaka alisema ripoti hiyo inaonyesha hali ya umaskini na ukosefu wa ajira duniani ni kubwa. Watu 205 milioni dunia kote mwaka 2010 hawakuwa na ajira.
Alisema idadi hiyo ilikuwa sawa na ongezeko la nguvu kazi isiyo na ajira duniani ya watu 27.7 milioni kulinganisha na ile ya mwaka 2007.
Alisema sababu za ongezeko la ukosefu wa ajira kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kutokana na utandawazi, maendeleo ya mawasiliano, mabadiliko ya teknolojia ambayo hayahitaji nguvu kazi nyingi katika utendaji kazi na kudidimia kwa nguvu za kiuchumi hasa katika nchi zinazoendelea.
Lowassa na ajira
Novemba 15, mwaka jana akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, Lowassa alionya kuhusu tatizo hilo na kulitaka lisaidie kujenga vyuo vya ufundi.
Alitoa takwimu akisema utafiti wa mwaka 2006, ambao hata hivyo, hakusema ulifanywa na taasisi gani, ulionyesha tatizo hilo kwa sasa limekuwa na kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvukazi ya taifa... “Ninapozungumza hili siyo nia yangu kumlenga mtu. Mimi ni Yohana Mbatizaji, hii ni sauti inayolia nyikani.”
Novemba 29, mwaka huo wa jana akiwa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKT), Usharika wa Amani Sabasaba, Singida, Lowassa alirudia tena suala hilo la tatizo ajira.
Mapema mwaka jana, Lowassa pia alifanya mkutano na waandishi wa habari Mjini Arusha na kuzungumzia tatizo hilo la ajira ambalo alilifananisha na bomu.
Jumatatu iliyopita, Lowassa alirejea kauli hiyo alipokuwa katika sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara akisema: “Nawaomba maaskofu katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la tatizo la ajira kwa vijana.... hili kama tulivyosema ni bomu linalosubiri kulipuka...”
March 21, 2012
Shirika la Umeme Tanzanian lapata mkopo kuzuia kukatika kwa umeme:
Benki tatu zimekubali kutoa mkopo wa shilingi bilioni 408 (Dola za Marekani 256) kwa Shirika la Umeme Tanzania kwaajili ya mpango wa dharula wa kuzuia kukatika kwa umeme, gazeti la Daily News la Tanzania liliripoti Jumatatu (tarehe 19 Machi).Fedha hizo zitasaidia kununua mafuta mazito kwaajili ya mitambo inayotumia mafuta mazito hayo, alisema William Mhando, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uzalishaji na Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO). "Tunatarajia kupata fedha hizo wili lijalo."
Kampuni inafanya kazi katika "changamoto ya muda" kukarabati miundombinu ya umeme nchi nzima, Mhando alisema, aliongeza kwamba uzalishaji umeshuka hadi megawati 718 kutoka megawati 1200. Alisema shirika la umeme halifanyi mgao wa umeme na tatizo lolote linatokana na mfumo mbaya wa miundombinu. "Hakukuwa na uwekezaji madhubuti katika eneo hili kwa muda mrefu," alisema.
City Bank Tanzania, National Microfinance Bank na National Bank of Commerce zinatoa mkopo kwaajili ya mradi huo.
Mwakyembe: Sijafa, nitabaki hai
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema waliokuwa wanataka kuandika kichwa cha habari kuwa amekufa sasa wajue yuko hai, na ametaka mjadala kuhusu kuugua kwake ufungwe kwa sababu umekuwa unaiumiza na kuiathiri sana familia yake.
Alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa katika makao makuu ya Wizara ya Ujenzi, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuripoti ofisini kwake kuendelea na kazi baada ya afya yake kuimarika kutokana na kuumwa kwa miezi kadhaa.
Dk.
 Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela (CCM), aliingia ofisini kwake jana 
saa 3.57 asubuhi na baadaye kuzungumza na waandishi kwa dakika 
zisizopungua 10, kuanzia saa 4.20 asubuhi.
Alisema
 mjadala kuhusu kuugua kwake, umekuwa ukishupaliwa na baadhi ya magazeti
 kwa kuupamba kwa vichwa vizuri vya habari ili kufanya biashara. 
“Lingine
 tu ambalo pengine waandishi wa habari niwaeleze, lakini niwaombe 
vilevile, jamani sasa suala la Mwakyembe kuumwa basi lifike basi 
mwisho,” alisema Dk. Mwakyembe, ambaye alirejea nchini Ijumaa iliyopita 
kutoka kwenye matibabu nchini India.
Aliongeza:
 “Unajua kwenye Journalism (uandishi wa habari) lazima mtu pia ujali 
hali inayowahusu watu wengine. Nina watoto. Sasa kila siku huyu baba 
ambaye anategemewa kufa kesho asubuhi hata kama inaleta headline (kichwa
 cha habari) kizuri kwenu na kuuza gazeti inaumiza.”
“Mliopenda
 kupata headline (kichwa cha habari) kwamba nimekufa, basi niko hai na 
nitaendelea kuwa hai. Kwa hiyo nawaombeni jamani yaishe tafadhali, 
nawaombeni sana,” alisema.
Alisema
 alikuwa anaumwa, lakini sasa amerudi kutoka nchini humo alikokuwa 
amekwenda kupata matibabu akiwa mzima na anaendelea na kazi.
“Nilikuwa
 naumwa, kwa kweli nimerudi sasa mimi ni mzima kabisa, naendelea na 
kazi, mmenikuta ofisini kwangu. Na sasa hivi ningependa nifanye kikao 
kiwe kifupi zaidi maana nina mafaili lundo yananisubiri kuweza 
kuyapitia,” alisema Dk. Mwakyembe.
AWASHUKURU JK, MAGUFULI, WATANZANIA
Aliishukuru
 serikali, hasa Rais Jakaya Kikwete, kwa kubeba jukumu hilo hadi kwenda 
kumuona nyumbani kwake na kushinikiza apata matibabu haraka 
iwezekanavyo.
Pia aliishukuru serikali kwa kuhakikisha amepata usafiri uliomuwezesha kwenda hospitali nchini India.
Vilevile,
 alimshukuru Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Katibu Mkuu, Balozi 
Herbert Mrango na Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk. John Ndunguru, kwa 
kuendesha wizara peke yao bila msaada wake.
Kadhalika, aliwashukuru wananchi wote nchini, wakiwamo Wakristo na Waislamu, waliojitolea kumuombea apate afya njema.
“Maombi yao hayakuwa ya bure, yamezaa matunda, mimi sasa hivi ni mzima na naendelea na kazi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Akijibu swali kwamba 
uchunguzi wa madaktari umeonyesha alikuwa akisumbuliwa na tatizo gani, 
alisema anaiachia serikali kupitia tume iliyoiunda kueleza suala hilo.  
“Kwa
 sababu nilipokuwa India nikaambiwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya 
Ndani ameunda tume inachunguza. Tuiache serikali. Kwa hiyo, kama kuna 
lolote ninalo nitaieleza serikali, na kama kuna taarifa yoyote nitaipa 
hii tume ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani amesema,” alisema Dk. 
Mwakyembe.
AWATAKA WAPIGAKURA KYELA
KUSITISHA MAANDAMANO
Aliwashukuru
 wapigakura wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, ambao walipanga kuandamana 
kwenda jijini Dar es Salaam kumuona Rais Kikwete ili waelezwe maradhi 
yaliyokuwa yanamsumbua Dk. Mwakyembe.
“Kwanza
 nitangulie kwa kuwashukuru sana. Kwanza kwa maombi yao na vilevile 
subira kubwa waliyokuwa nayo katika kipindi chote ambacho mbunge wao 
nimekuwa sipo,” alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza:
 “Naomba niwahakikishie tu wana Kyela hawana haja ya kuandamana tena, 
nimekuja. Napanga kwenda Kyela mimi mwenyewe katika wiki moja mbili 
zijazo kufuatana na lundo la kazi litakalopungua hapa wizarani.”
Kuhusu
 kupishana kauli kati yake na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
 (DCI), Kamishna Robert Manumba, Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa hawezi 
kurejea tena suala hilo kwa vile linashughulikiwa na serikali. 
“Serikali
 imeamua kulichunguza hili suala. Sasa hatuwezi kuendesha parallel 
systems (mifumo sambamba). Serikali inachunguza halafu sisi huku kama 
waandishi wa habari tunaongea haya, haitokuwa sahihi,” alisema Dk. 
Mwakyembe. 
Aliongeza:
 “Tuiache serikali iangalie hili suala, maana nikisema serikali ni 
pamoja na hata yeye DCI Manumba, polisi wote wanahusika. Kwa hiyo, hebu 
tuipe nafasi serikali ije na taarifa ambayo pengine itaturidhisha wote.”
“Lakini kwa upande wangu mimi kama Mwakyembe, mimi kama nilivyosema siku nyingi namuachia Mungu. Na tuiachie serikali.”
‘UGONJWA WAKE NI WA KITAALAMU’
Alisema hawezi kuwaeleza Watanzania ugonjwa unaomsumbua hawataelewa kwa sababu ni mambo ya kitaalamu.
“Hata kama watu watakimbilia kuuangalia (ugonjwa huo) kwenye kamusi hawawezi kufanikiwa kupata chochote,” alisema Dk. Mwakyembe.
Dk.
 Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9, 
mwaka jana, yalimlazimu kupelekwa katika Hospitali ya Appolo, India kwa 
matibabu zaidi.
Maradhi
 hayo yalizua utata mkubwa baada ya kudaiwa kuwa yametokana na kuwekewa 
sumu, huku kukiwa na kauli mbalimbali zinazotofautiana kutoka kwake na 
baadhi ya watendaji wengine wa serikali.
Kauli
 tata zaidi ziliibuka baada baadhi ya viongozi, akiwamo Waziri wa 
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, kudai kuwa maradhi 
yanayomsumbua Dk. Mwakyembe yametokana na kulishwa sumu.
Hata
 hivyo, Kamishna Manumba alijibu madai hayo aliposema kuwa uchunguzi wa 
polisi umebaini kuwa Dk. Mwakyembe hajaugua kwa sababu ya kulishwa sumu 
na kutishia kuwachukulia hatua waliotoa kauli hizo.
Ripoti
 ya uchunguzi aliyoisoma Manumba katika mkutano wake na waandishi wa 
habari Februari 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, inaonyesha kuwa Dk.
 Mwakyembe hakulishwa sumu huku akisema kwamba pia ilijumuisha taarifa 
kutoka hospitalini India ambako alikuwa anatibiwa.
Alisema
 uchunguzi huo unalipa Jeshi la Polisi picha kuwa waliotoa taarifa hizo 
hadharani wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baada
 ya kauli hiyo, Dk. Mwakyembe aliibuka na kutoa kauli nzito iliyoonekana
 kumjibu Kamishna Manumba akielezea kushangazwa kwake na majibu hayo, 
huku akisisitiza kuwa madaktari waliokuwa wakimtibu walikuwa wakitafiti 
chanzo cha  ugonjwa wake na walikuwa hawajafikia hitimisho, hivyo si 
sahihi kwa Manumba kusema kuwa hautokani na kulishwa sumu, kwani sumu si
 lazima ikudhuru kwa kulishwa tu.
Mbali
 ya Dk. Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, 
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa nyakati 
tofauti walikana kuijua ripoti hiyo ya Kamishna Manumba.
Hata
 hivyo, katika kile kilichoonekana kudhamiria kuchukua hatua, Kamishna 
Manumba aliwasilisha jalada la mashtaka kwa watu hao kwa Mkurugenzi wa 
Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, ambaye alithibitisha kupokea jalada 
hilo, lakini alisema ni vigumu kufahamu ni lini atakapopeleka mahakamani
 jalada la kesi dhidi ya watu hao.


 
 

